Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, amemteua rasmi Pius Mwandu Lukanula kuwa Katibu wake, hatua inayotafsiriwa kama kuendelea kuimarisha uwajibikaji na uratibu wa huduma kwa wananchi wa jimbo hilo.
Uteuzi huo umetangazwa hadharani Januari 21, 2026, katika kikao cha kuwasilisha taarifa Wilaya ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2025. Tangazo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kishapu, Shija Ntelezu, katika ukumbi wa mikutano wa chama hicho wilayani hapo.
Akizungumza mbele ya wajumbe na viongozi wa chama, Ntelezu amesema uteuzi wa Mwandu umetokana na maelekezo ya moja kwa moja kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu.
“Kutokana na maelekezo kutoka kwa Mbunge wetu, kuanzia leo Pius Mwandu anatambulika rasmi kuwa Katibu na msaidizi wake. Hivyo, kero na changamoto mbalimbali za wananchi zinazopaswa kufikishwa kwa Mbunge, endapo atakuwa hayupo, zitapokelewa na kushughulikiwa na Pius kwa niaba yake,” amesema Ntelezu.
Kwa upande wake, Pius Mwandu, mara baada ya kutangazwa rasmi, amemshukuru Mhe. Lucy Mayenga kwa kumuamini na kumpa jukumu hilo zito la uongozi, akiahidi kulitumikia kwa uadilifu, weledi na uzalendo mkubwa kwa maslahi ya wananchi wa Kishapu.
“Naomba nipate ushirikiano kutoka kwa wanachama wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi pamoja na watendaji wa Serikali ili kwa pamoja tuweze kuwahudumia wananchi wetu kwa ufanisi,” amesema Mwandu.
KIUFUPI PIUS MWANDU NI NANI?
Pius Mwandu alizaliwa miaka ya 1990 katika Kijiji cha Mwamadulu, Kata ya Lagana, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Ni kijana anayejishughulisha na shughuli za kilimo na ujasiriamali, huku akijipambanua kama mmoja wa vijana wenye mchango mkubwa ndani ya chama na jamii kwa ujumla.
ELIMU
-Mwamadulu Shule ya Msingi, Kishapu (Elimu ya Msingi)
-Mkungi Shule ya Sekondari, Kibaha (Kidato cha 1-4)
-Matai High School , Rukwa (Kidato cha 5&6)
-Chuo Kikuu cha Dar es salam
UZOEFU WA UONGOZI
Katika safari yake ya uongozi, Mwandu amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo:
-Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
-Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Wilaya ya Kishapu
Uteuzi wa Pius Mwandu unaendelea kuashiria dhamira ya Mbunge wa Jimbo la Kishapu ya kuwapa nafasi vijana wenye uwezo na uzoefu katika kuwatumikia wananchi na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya maendeleo jimboni.Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Shija Ntelezu akimtangaza rasmi Katibu wa Mbunge wa Jimbo hilo, Pius Mwandu Lukanula kwenye kikao cha uwasilishaji taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ngazi ya wilaya katika ukumbi wa mikutano wa Chama hicho Januari, 21,2026
Post a Comment