Na Sumai Salum – Kishapu
Jumla ya miti 1,500 imepandwa katika Shule ya Msingi Isoso, Kata ya Kishapu Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kama sehemu ya kuenzi mchango na maono ya Rais Samia katika kulinda na kuhifadhi mazingira nchini.
Akizungumza mnamo Januari,27,2026 kwa niaba ya Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Fatma H. Mohammed, amesema upandaji wa miti ni nguzo muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda vyanzo vya maji pamoja na kuhakikisha mustakabali salama wa mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Fatma ameeleza kuwa maadhimisho hayo yamebeba ujumbe mzito wa kuendeleza maono ya Rais Samia ya Tanzania ya kijani, akibainisha kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki kikamilifu katika upandaji na utunzaji wa miti.
“Kupanda mti mmoja leo ni kuwekeza maisha ya kesho. Tunapaswa kupanda, kutunza na kulinda miti kwa faida ya Taifa letu,” amesema Bi. Fatma.
Kwa upande wake Mhifadhi Misitu Wilayani Kishapu Tumaini Masatu, amesema TFS imeendelea kuwa kinara katika juhudi za uhifadhi wa misitu na mazingira kwa kutekeleza kampeni za upandaji miti na kutoa elimu ya uhifadhi, hususan kwa wanafunzi ili kujenga kizazi chenye uelewa, uzalendo na uwajibikaji wa kimazingira.
Mhifadhi Misitu Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Tumaini Masatu akizungumza kwenye zoezi a upandaji miti 1,500 katika Shule ya Msingi Isoso, Kata ya Kishapu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Januari 27,2026
Masatu amefafanua kuwa miti iliyopandwa katika shule hiyo itachangia kuboresha mazingira ya kujifunzia, kutoa kivuli, matunda, kupunguza athari za ukame pamoja na kuwajengea wanafunzi uelewa wa vitendo kuhusu umuhimu wa rasilimali za misitu.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Isoso Mwl. Gilbert Mtunguja ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Kishapu na TFS kwa kuchagua shule hiyo kuwa sehemu ya maadhimisho hayo muhimu, akiahidi kuwa uongozi wa shule kwa kushirikiana na wanafunzi utahakikisha miti yote iliyopandwa inatunzwa na kulindwa ipasavyo.
Kwa upande wao, wanafunzi wa shule hiyo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyoipata kuhusu utunzaji wa mazingira, wakiahidi kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira shuleni na katika jamii zao.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa zoezi la pamoja la upandaji miti likiwahusisha viongozi,wakuu wa Taasisi, watumishi wa Halmashauri, TFS, walimu, wanafunzi na wananchi, ikiwa ni ishara ya mshikamano na dhamira ya dhati ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda na kuhifadhi mazingira nchini yakiambatana na kauli mbiu isemayo "Uzalendo ni kulinda mazingira, shiriki kupanda miti".
Post a Comment