SOUWASA YANG’ARA WIKI YA MAJI SONGEA YAWATUNUKIA WATEJA BORA NA KUHAMASISHA ULIPAJI ANKARA KWA WAKATI

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imeendeleza maadhimisho ya Wiki ya Maji kwa vitendo, kwa kuwatunukia tuzo wateja wake bora katika makundi matatu ambayo ni wateja wa majumbani, biashara na taasisi. 

Utoaji wa tuzo hizo umefanyika leo Machi 19, 2026 katika maeneo tofauti ya mji wa Songea, ikiwemo Chuo cha Ualimu Songea (TTC), ikiwa ni sehemu ya kuthamini ushirikiano wa wateja katika kuboresha huduma ya maji.

Akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja Baby Bicco, amesema kuwa katika kipindi cha Wiki ya Maji, mamlaka hiyo imeendesha shughuli mbalimbali ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira pamoja na uelimishaji kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. 

"Ndugu zangu, utoaji wa tuzo hizo ni sehemu ya kuwatambua na kuwahamasisha wateja wanaolipa Ankara kwa wakati na kutumia huduma kwa uwajibikaji" ameongeza 

Bicco amebainisha kuwa vigezo vilivyotumika kupata washindi ni pamoja na matumizi makubwa ya maji yanayoendana na ulipaji mzuri wa Ankara kwa wakati katika makundi yote matatu. 

 Aidha, amesema SOUWASA pia imetoa tuzo maalum kwa mdau wa maji aliyekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za uharibifu wa miundombinu, wizi wa mita na uvujaji wa mabomba, jambo lililosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Songea, Bi Catherine Thomas Kimboka, ambaye ni miongoni mwa waliopokea tuzo, amesema taasisi yake imekuwa mnufaika mkubwa wa huduma ya maji kutoka SOUWASA.

Ameeleza kuwa upatikanaji wa maji wa uhakika umewezesha chuo chenye zaidi ya wanafunzi 400 kudumisha usafi wa mazingira na kuepuka magonjwa ya mlipuko. Amehimiza taasisi nyingine kuhakikisha zinalipa Ankara kwa wakati ili kusaidia mamlaka kuendelea kutoa huduma bora.

 Nao baadhi ya wapokeaji wa tuzo, wakiwemo Ibrahim Khakimu Faraji kwa niaba ya wenzake, wameishukuru SOUWASA kwa utambuzi huo na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za hitilafu za miundombinu ya maji. 

 Pia wamewataka wateja kulipa bili kwa wakati na kuhakikisha miundombinu ya ndani ya majumba yao yapo imara ili kuepuka bili kubwa zisizo za lazima, huku akionya kuwa kuchelewa kulipa kunaweza kusababisha huduma ya maji kukatwa.

 

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post