SOUWASA YAPANDA MITI 500 KULINDA VYANZO VYA MAJI SONGEA, WIKI YA MAJI YAADHIMISHWA KWA VITENDO


Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa SOUWASA, Bi Baby Bicco akishiriki zoezi la upandaji miti katika kuadhimisha wiki ya Maji inayoendelea kitaifa kuanzia Machi 16 hadi 22 kwa kufanya zoezi la upandaji miti katika bonde la Mto Luhila, lililopo kata ya Seedfarm, Manispaa ya Songea mkoani humo Machi 18,2026

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imeadhimisha Wiki ya Maji inayoendelea kitaifa kuanzia Machi 16 hadi 22 kwa kufanya zoezi la upandaji miti katika bonde la Mto Luhila, lililopo kata ya Seedfarm, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.


Katika maadhimisho hayo, miti 500 imepandwa ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda vyanzo vya maji vinavyotegemewa na wakazi wa manispaa hiyo.


Mgeni rasmi katika tukio hilo, Meya wa Manispaa ya Songea, Mheshimiwa Abraham Egno Mbunda, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kampeni ya upandaji miti, akiwataka madiwani kupewa elimu maalum ili kusimamia zoezi hilo katika kata zao.


Amesema baadhi ya maeneo yamekuwa na upungufu mkubwa wa miti hali inayochangia uharibifu wa mazingira, na kusisitiza kuwa ni wakati sasa kwa viongozi kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.


Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa SOUWASA, Mhandisi Jafari Kinjalambaya, amesema kuwa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Manispaa ya Songea imekuwa ikiendesha zoezi la upandaji miti kila mwaka kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji.


Ameeleza kuwa Mto Luhila ndio chanzo kikuu cha maji kwa manispaa hiyo, hivyo juhudi za kulinda mazingira yake ni muhimu.


Aidha, amesema katika kipindi hiki cha Wiki ya Maji, wamekuwa wakitoa elimu kupitia vyombo vya habari pamoja na kuhimiza wananchi kuepuka uchomaji holela wa misitu unaoharibu vyanzo vya maji.


Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa SOUWASA, Bi Baby Bicco, amebainisha kuwa maadhimisho ya Wiki ya Maji huambatana na shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji miti, akisisitiza kuwa maji ni rasilimali muhimu inayohitaji kulindwa kwa vitendo.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya Wiki ya Maji ni “Maji na Jinsia”, ikilenga kuhamasisha usawa na ushirikishwaji wa jamii nzima katika usimamizi wa rasilimali za maji.

Meya wa Manisipaa ya Songea Mkoani Ruvuma Mhe. Abraham Egno Mbunda, akishiriki zoezi la upandaji miti 500 lililoandaliwa na kuratibiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) katika kuadhimisha wiki ya Maji inayoendelea kitaifa kuanzia Machi 16 hadi 22 kwa kufanya zoezi la upandaji miti katika bonde la Mto Luhila, lililopo kata ya Seedfarm, Manispaa ya Songea mkoani humo Machi 18,2026
Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa SOUWASA, Mhandisi Jafari Kinjalambaya akishiriki zoezi la upandaji miti katika kuadhimisha wiki ya Maji inayoendelea kitaifa kuanzia Machi 16 hadi 22 kwa kufanya zoezi la upandaji miti katika bonde la Mto Luhila, lililopo kata ya Seedfarm, Manispaa ya Songea mkoani humo Machi 18,2026







0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post