UWEKEZAJI ELIMU KWA WASICHANA NI KUJENGA TAIFA IMARA- MBUNGE MAYENGA

Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe. Lucy Thomas Mayenga akizungumuzia kuhusu umuhimu wa kuwekeza elimu kwa mtoto wa kike alipokuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Tamasha la amani na maendeleo lililoanza Februari 23 hadi Februari 28,2026 kwenye viwanja vya shule ya msingi Buduhe iliyoko kataya Kishapu wilayani Kishapu

Na sumai Salum- Kishapu



Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Mhe. Lucy Mayenga, ametoa wito kwa jamii kuwekeza zaidi katika elimu, hususan kwa watoto wa kike, akisisitiza kuwa elimu ni msingi imara wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Akizungumza katika kilele cha Tamasha la Amani na Maendeleo lililofanyika katika viwanja vya michezo Shule ya Msingi Buduhe wilayani Kishapu  mkoani Shinyanga, ameeleza kuwa uwekezaji katika elimu ya mtoto wa kike ni hatua muhimu ya kupunguza umasikini, utegemezi, mimba na ndoa za utotoni.


Mhe. Mayenga amesema kuwa, jamii inapaswa kubadili mtazamo potofu unaowakwamisha wasichana kupata elimu bora, akibainisha kuwa mtoto wa kike akipata elimu anakuwa chachu ya maendeleo katika familia na jamii kwa ujumla.


 “Elimu kwa mtoto wa kike si hisani, ni haki yake ya msingi. Tukimuelimisha msichana, tumeielimisha jamii nzima,” amesisitiza.


Aidha, amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya kwenda shule na kumaliza masomo yao bila vikwazo vya kijamii au kiuchumi. Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya shule, kuongeza walimu na kuimarisha mazingira rafiki ya kujifunzia ili kila mtoto aweze kufikia ndoto zake.


Katika tamasha hilo lililolenga kuhimiza amani, mshikamano na maendeleo, wananchi walikumbushwa kuwa elimu inaleta manufaa mengi ikiwemo kuongeza ajira, kuboresha afya ya familia, kukuza uchumi wa kaya na taifa, pamoja na kuimarisha maadili na uwajibikaji katika jamii.


Mbunge huyo amehitimisha kwa kuwataka wadau wa maendeleo, taasisi binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana na Serikali katika kuwekeza kwenye miradi ya elimu, hasa ile inayowalenga wasichana, ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo.


Tamasha la Amani na Maendeleo limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha viongozi na wananchi kujadili masuala ya kijamii na kiuchumi, huku suala la Elimu na Bima ya afya kwa watu wote ikipewa kipaumbele kama nguzo kuu ya ustawi wa Taifa.





0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post