TANFORD YATANGAZA KONGAMANO LA KIMATAIFA DUBAI KUFUNGUA FURSA ZA BIASHARA KWA TANZANIA
0
Na Mwandishi Wetu
Umoja wa Wawakilishi wa Mawakala wa Usafirishaji wa Mizigo wa Tanzania waliopo Dubai ujulikanao kama Tanzania Freight Forwarders Representation in Dubai (TANFORD) umetangaza kuandaa kongamano la kimataifa la siku mbili litakalofanyika jijini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa lengo la kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa na kufungua fursa mpya za biashara kwa wafanyabiashara wa Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TANFORD, Bw. Hussein Jamal, amesema kongamano hilo linalojulikana kama Tanzania Trade and Logistics Forum 2026 litafanyika tarehe 13 na 14 Februari, 2026, na linatarajiwa kuwakutanisha wadau wa sekta ya biashara, usafirishaji na logistics kutoka mataifa mbalimbali.
Bw. Jamal amesema kongamano hilo lina lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa na kuifanya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati, sambamba na kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji ya Tanzania kwa kukusanya mizigo kutoka masoko ya kimataifa kupitia nchi hiyo.
Ameeleza kuwa kupitia kongamano hilo, wafanyabiashara wa Kitanzania watapata fursa ya kukutana ana kwa ana na wateja wa kimataifa, jambo litakalosaidia kufungua masoko mapya ya bidhaa za Tanzania na kuimarisha uhusiano wa kibiashara.
“TANFORD inasimama kama daraja la kibiashara kati ya Tanzania na masoko ya kimataifa, kwa lengo la kuwasaidia Watanzania kutambua na kutumia fursa za biashara na usafirishaji zilizopo Dubai, pamoja na kutangaza biashara zao kimataifa,” amesema Jamal.
Ameongeza kuwa kongamano hilo ni fursa adhimu kwa wadau wa sekta binafsi, taasisi za serikali pamoja na makampuni ya usafirishaji, likiwa na manufaa makubwa kwa mtu mmoja mmoja, makampuni na taifa kwa ujumla.
Taasisi zinazotarajiwa kushiriki katika kongamano hilo ni pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), DP World, TAFFA, TANTRADE, TATOA, Port Marine Clearing & Forwarding, Silent Ocean, Kilimanjaro Star Cargo pamoja na TPSF.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, amesema ushiriki wa Tanzania katika makongamano ya kimataifa ni muhimu kwani huimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara wa ndani na wa kimataifa.
“Nawasihi wafanyabiashara wa Kitanzania kushiriki kongamano hili kwani litafungua fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali,” amesema Dkt. Latifa.
Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edwin Urio, amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kujitangaza kibiashara, kujijengea uwezo na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.
Ameeleza kuwa sekta ya logistics na usafirishaji ndiyo iliyoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini katika mwaka wa fedha 2024/2025, na kuendelea kuwa uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi wa taifa lolote.
Bw. Urio pia amepongeza ushirikiano kati ya taasisi za serikali na sekta binafsi katika kuandaa kongamano hilo, akisema ushirikiano huo una mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
إرسال تعليق