Na Sumai Salum- Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi, leo Februari 27,2026 amezindua rasmi mpango wa Bima ya Afya kwa watu wote wilayani humo, hafla iliyofanyika katika viwanja vya michezo vya Shule ya Msingi Buduhe Kata ya Kishapu.
Uzinduzi huo umeenda sambamba na uhamasishaji mkubwa kwa wananchi kujiunga na mpango huo muhimu wa kitaifa unaolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila ubaguzi.Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza kwenye Tamasha la Amani na Maendeleo Kishapu wakati akizindua Rasmi Mpango WA Bima ya afya kwa wote ngazi ya Wilaya kwenye viwanja vya michezo Shule ya Msingi Buduhe Kata ya Kishapu Wilayani humo Februari 27,2026
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Masindi amesema kuwa jumla ya Wananchi 11,535 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo katika wilaya ya Kishapu, sawa na wastani wa Kaya 2,257 na mchango wa shilingi 150,000 kwa kila kaya kwa mwaka.
Mhe. Masindi amesisitiza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan, ambaye analenga kuleta usawa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote, wenye uwezo na wasio na uwezo.
“Dhamira ya Serikali ni kuona kila mwananchi anapata matibabu bora bila kujali hali yake ya kipato. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameleta mpango wa Bima ya Afya kwa watu wote ili kuhakikisha usawa na haki katika sekta ya afya,” amesema Mhe. Masindi.
Aidha, amewataka viongozi wa Kata, Vijiji na mitaa kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kuhakikisha wanajitokeza kujiunga na mpango huo, huku akisisitiza kuwa afya ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo wamepongeza juhudi za Serikali kwa kuanzisha mpango huo, wakieleza kuwa utasaidia kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kuanzia Zahanati, Vituo vya afya, Hospitali za Mkoa hadi Hospitali za Rufaa nchi Tanzania.
Post a Comment