
Akizungumza na mamia ya wananchi waliojitokeza kwa shangwe na nderemo, Mheshimiwa Mayenga alieleza kuwa ushindi wake ni ushindi wa wananchi wote wa Kishapu, na akaahidi kuendelea kuwatumikia kwa uadilifu, uwazi na juhudi zisizochoka.
Katika kuonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kuwaletea maendeleo wananchi, Mheshimiwa Mbunge ameahidi kuwa ndani ya wiki ijayo atawakabidhi wananchi wa Kijiji cha Ijimija kiasi cha shilingi milioni mbili (2,000,000/=) kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho. Hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi na kupunguza adha ya kufuata matibabu umbali mrefu.
Aidha, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Ofisi ya Chama cha Mapinduzi Kata ya Shagihilu, Mheshimiwa Mayenga ameahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni moja (1,000,000/=) ili kuhakikisha ofisi hiyo inakamilika kwa wakati na kuendelea kuwa kitovu cha uratibu wa shughuli za maendeleo na siasa katika kata hiyo.
Katika hatua nyingine ya kutia moyo, jioni ya leo wananchi wa Ijimija wamekabidhiwa rasmi ramani ya zahanati, hatua inayofungua rasmi pazia la kuanza kwa ujenzi mara moja.
Kwa vitendo hivi, Mheshimiwa Lucy Mayenga ameendelea kudhihirisha kuwa Mbunge ni sauti ya wananchi. Amechagua kuishi kauli hiyo kwa matendo — akisimama bega kwa bega na wananchi wake, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.


Post a Comment