MHE. MWIJUMA AZINDUA MKUTANO WA UTANGAZAJI DODOMA, ADA YA VYOMBO VYA HABARI MTANDAONI YAPUNGUA

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Februari 12,2026 ukumbi wa New Generation Kisasa Jijini Dodoma


Na Sumai Salum – Dodoma


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka kwa Sekta ya Utangazaji utakaofanyika Februari 12–13, 2026 katika Ukumbi wa New Generation, Kisasa jijini Dodoma, wenye lengo la kujadili mustakabali wa sekta hiyo hususan namna teknolojia inavyoweza kupanua na kuboresha huduma za utangazaji vijijini.

Mkutano huo umebeba kauli mbiu isemayo “Matumizi ya Teknolojia katika Kupanua na Kuboresha Huduma za Utangazaji Vijijini,” ikilenga kuhamasisha wadau wa sekta ya utangazaji kutumia ubunifu na mifumo ya kidijitali kuwafikia wananchi walioko maeneo ya pembezoni mwa nchi.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwijuma, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia katika sekta ya utangazaji ili kuhakikisha huduma zinawafikia Watanzania wote bila kujali walipo.


"Hata sasa Serikali imechukua hatua kubwa ya kuipumua sekta ya habari mtandaoni baada ya kupunguza kwa kiwango kikubwa ada za maombi ya leseni. Ada hiyo sasa imeshuka kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000, huku ada ya maombi ikipunguzwa kutoka 50,000 hadi 10,000 — hatua inayotajwa kufungua ukurasa mpya kwa wanablogu na wamiliki wa majukwaa ya kidijitali nchini" ameongeza Mwijuma


Mbali na punguzo hilo, Mwinjuma ameielekeza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kuhakikisha wafanyakazi wa vyombo vya habari wanapatiwa mishahara na stahiki zao kwa wakati. Amesisitiza kuwa madai ya wafanyakazi wanaodai mishahara ya zaidi ya miezi mitano hayapaswi kuendelea, na ametaka mrejesho wa utekelezaji huo ndani ya wiki moja.


pamoja na hayo ameongeza kuwa maendeleo ya teknolojia yamefungua fursa mpya kwa vituo vya redio na televisheni kupanua wigo wa usikivu na utazamaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, ubora wa maudhui na uzalendo katika utoaji wa habari.


Akiweka msisitizo katika dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwinjuma amesema maboresho ya mazingira ya kazi kwa vyombo vya habari yataendelea kutekelezwa, huku akihimiza uzalishaji wa maudhui bora, yanayozingatia maadili ya taaluma na kulinda haki miliki.


“Haki ya kupata taarifa ni ya kila Mtanzania. Vyombo vya habari vina wajibu wa kuhakikisha vinawafikia wananchi wote bila ubaguzi,” ameeleza.


Mkurugenzi mkuu TCRA Dkt. Jabiri Bakari ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa wadau kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utangazaji, ikiwemo gharama za uendeshaji, matumizi ya mifumo ya kidijitali na namna ya kuongeza ushiriki wa jamii katika uzalishaji wa maudhui huku akiwasilisha takwimu za vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini na kuahidi kuimarisha miundombinu ya mawasiliano kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


Wadau mbalimbali wa utangazaji kutoka mikoa tofauti nchini wamehudhuria mkutano huo, wakijadiliana kwa kina mikakati ya kuimarisha huduma za utangazaji vijijini ili ziwe chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa kwa maazimio yatakayosaidia kuimarisha sekta ya utangazaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Taifa
.Mkurugenzi mkuu TCRA Dkt. Jabiri Bakari akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa vyombo vya utangazaji ambapo Mgeni Rasmi akiwa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwijuma Februari 12,2026 ukumbi wa New Generetion Kisasa Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post