Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga Mhe. Julius Sunday Mtatiro akizungumza Machi 18, 2026 katika hafla ya futari (Iftar) iliyoandaliwa na TAKUKURU mkoani humo
Na Estomine Henry- Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga Mhe. Julius Sunday Mtatiro, amewataka wananchi kuongeza ushirikiano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuimarisha haki na kuchochea maendeleo ya taifa.
Akizungumza Machi 18, 2026 katika hafla ya futari (Iftar) iliyoandaliwa na TAKUKURU mkoani Shinyanga, Mtatiro amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi.
Ameeleza kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo kwani husababisha upotevu wa rasilimali za taifa, akibainisha kuwa vitendo hivyo vinahusisha pande zote mbili—wanaotoa na wanaopokea rushwa.
“Mapambano ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinasimamiwa kwa uadilifu na kunufaisha wote,” alisema Mtatiro.
Aidha, amebainisha kuwa changamoto ya ukosefu wa maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma imekuwa ikichangia kuwepo kwa vitendo vya rushwa, hali inayosababisha wananchi kunyimwa haki zao.
“Mashauri mengi ya kesi yanaonesha wazi kuwa kuna upotoshaji wa ukweli kwa ajili ya kupata au kutoa rushwa ili kujinufaisha binafsi kwa kumdhulumu mwingine,” ameongeza.
Mtatiro aliwataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa TAKUKURU, akisisitiza kuwa taasisi hiyo imejipanga kupokea na kufanyia kazi taarifa hizo kwa ufanisi.
Amepongeza TAKUKURU kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma pamoja na kufanikisha ushiriki mkubwa wa wananchi katika hafla hiyo, akisema ni ishara kuwa jamii imeanza kuelewa umuhimu wa kupinga rushwa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amegusia juhudi za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa wilayani humo, hususan katika sekta ya afya, na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi.
.png)

.png)




إرسال تعليق