DTO KAHAMA ATOA MAFUNZO KWA MADEREVA WA SERIKALI

Na Mwandishi wetu- Polisi


Madereva wa Serikali katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama wamepatiwa mafunzo maalum ya usalama barabarani yaliyolenga kuongeza uelewa na kuwajengea nidhamu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.


Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na kutolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kahama, Mrakibu wa Polisi (SP) Flora Nangawe, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kupunguza ajali zisizo za lazima.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, SP Nangawe amewataka madereva kuhakikisha hawaendeshi magari wakiwa na leseni zilizokwisha muda wake, akieleza kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria na linaweza kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.


Aidha, amekemea vikali tabia ya unywaji wa pombe wakati wa uendeshaji wa vyombo vya moto, akibainisha kuwa ulevi hupunguza umakini na kuongeza hatari ya ajali. “Dereva anatakiwa kuwa makini muda wote anapokuwa barabarani, na si vinginevyo,” alisisitiza.


Katika hatua nyingine, SP Nangawe amewahimiza madereva hao kuheshimu na kutii amri zote wanazopewa na askari wa usalama barabarani, pamoja na kufuata alama na ishara za barabarani, ambazo zimewekwa kwa lengo la kulinda maisha ya watu na mali zao.


0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم