KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YARIDHISHWA NA MRADI WA UMEME WA JUA KISHAPU



Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Nishati na Madini Subira Mgalu akizungumza.

Na Kadama Malunde - Shinyanga


Katika hatua ya kuimarisha uzalishaji wa nishati safi na kuongeza uwezo wa gridi ya taifa, awamu ya kwanza ya mradi wa umeme wa jua wa Kishapu mkoani Shinyanga imekamilika na kuanza kuzalisha megawati 50 ambazo tayari zimeingizwa kwenye mfumo wa umeme wa taifa.


Kukamilika kwa mradi huo kumepokelewa kwa kuridhishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyotembelea mradi huo pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli kilichopo Manispaa ya Shinyanga.


Akizungumza leo Machi 13, 2026 wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi wa umeme wa jua wa Kishapu pamoja na kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli kilichopo Manispaa ya Shinyanga, Mwenyekiti wa kamati hiyo Subira Mgalu, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.


“Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa mradi huu wa umeme wa jua. Tunafarijika kwamba megawati hizi 50 tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa,” amesema Mgalu.


Aidha, ameishauri serikali kuanza mapema utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo itakayozalisha megawati 100 ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini na kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme.


Akizungumza kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, ameipongeza serikali kwa kutumia fedha zake za ndani sh.bilioni 207 kwa ajili ya kupanua kituo hicho.


Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema mradi wa umeme wa Jua wilayani Kishapu, ulianza kutekelezwa mwaka 2023 na awamu ya kwanza umekamilika kwa kuzalisha megawati 50 ambazo tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa.


Amesema, ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo umegharimu Sh. bilioni 118.


“Megawati hizi 50 ni awamu ya kwanza, sasa tunajiandaa kuanza awamu ya pili ambayo itazalisha megawati 100 kwa gharama ya sh. bilioni 216 na tupo katika hatua za kumpata mkandarasi,” amesema Ndejembi.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati, ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika utakaochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.


Kwa upande wake, Meneja wa mradi wa umeme wa jua wa Kishapu Emmanuel Anderson, amesema mradi huo una jumla ya paneli za sola 82 na zinatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 25.






Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi akizungumza.























0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم