MAADHIMISHO YA SIKU YA MISITU KANDA YA MAGHARIBI YAFANYIKA SHINYANGA, HEKTA 469,000 HUPOTEA KILA MWAKA


Na Sumai Salum – Shinyanga

Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi umeadhimisha Siku ya Misitu Duniani kwa kufanya mazungumzo na waandishi wa habari pamoja na kupanda miti 300 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Machi 20, 2026 katika ofisi za TFS wilayani Shinyanga, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Said Kitinga, ameupongeza wakala huo kwa jitihada zake za kusimamia kwa ufanisi sera za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika kampeni ya upandaji miti.


Amesema serikali imetoa ruzuku kwa ajili ya matumizi ya nishati safi, ikiwemo gesi, na pia imeielekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linakuja na mbadala wa majiko banifu ili wananchi waweze kuyapata kwa gharama nafuu, hatua itakayosaidia kulinda mazingira.


“Serikali pia imeagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapanda miti katika taasisi za umma, ambapo lengo ni kufikia miti takribani milioni 1.5 kwa kila mwaka. Tayari tunaona matokeo yake, hususan katika shule na magereza ambako matumizi ya nishati safi na majiko banifu yameanza kuimarika,” amesema Kitinga.


Aidha, ameipongeza TFS kwa usimamizi mzuri wa misitu na hifadhi mbalimbali walizokabidhiwa, akibainisha kuwa ulinzi umeimarika na uvamizi umepungua. Amewataka kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi ambaye pia ni Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda, Shadrack Msilu, amesema lengo kuu la wakala huo ni kurejesha uoto wa asili kupitia upandaji miti.


Amesema takwimu zinaonesha kuwa Tanzania Bara hupoteza takribani hekta 469,000 za misitu kila mwaka kutokana na ukataji wa miti bila kupanda mingine.


Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kufika katika ofisi za TFS zilizopo maeneo yao ili kupata elimu ya uhifadhi wa misitu, akisisitiza kuwa uhifadhi huo unaweza pia kuwa chanzo cha kipato na kusaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja.


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga, Mwl. Nurah Wirfred Kamuntu, amesema shule hiyo inanufaika na uwekezaji mkubwa wa miundombinu, hivyo uwepo wa miti ni muhimu kwa ajili ya vivuli, hewa safi na mazingira rafiki kwa wanafunzi.


“Kama mlivyoona, tuna wanafunzi 856 na hadi sasa tuna miti 5,974, sawa na wastani wa miti 14 kwa kila mwanafunzi. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na miti angalau 20,” amesema Kamuntu.


Maadhimisho hayo yamehusisha mikoa minne ya Kanda ya Magharibi ambayo ni Shinyanga, Tabora, Katavi na Kigoma, na yamefanyika mkoani Shinyanga yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Misitu ni Uchumi, Tuhifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.”

Katibu Tawala wilayani Shinyanga mkoani Shiyanga, Said Kitinga  akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Misitu Duniani ya Wakala wa misitu Tanzania TFS Kanda ya magharibi yaliyofanyika katika ofisi za Wilaya hiyo Machi 20, 2026 
Mwakilishi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Magharibi ambaye pia ni Afisa Misitu Mwandamizi na Mkuu wa Operesheni Kanda, Shadrack Msilu,  akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Misitu Duniani ya Wakala wa misitu Tanzania TFS Kanda ya magharibi yaliyofanyika katika ofisi za Wilaya ya Shinyanga Machi 20, 2026 
Mhifadhi Mwandamizi  kutoka wakala wa misitu TFS wilayani Shinyanga mkoani Shiyanga, Fabian Balele akifuatilia uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Misitu Duniani ya Wakala wa misitu Tanzania TFS Kanda ya magharibi yaliyofanyika katika ofisi za Wilaya hiyo Machi 20, 2026 
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga iliyoko mtaa wa Butegwa Kata ya ndebezi Wilayani Shinyanga mkoani Shinyanga, Mwl. Nurah Wirfred Kamuntu, akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Misitu Duniani ya Wakala wa misitu Tanzania TFS Kanda ya magharibi yaliyofanyika katika ofisi za Wilaya ya Shinyanga Machi 20, 2026 
Mratibu wa waandishi wa habari mkoani Shinyanga Estomine Henry akizungumza















































































0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post