
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imeendelea kuthibitisha ubora wake katika utoaji wa huduma baada ya kushika nafasi ya pili kitaifa miongoni mwa mamlaka 20 za maji zenye wateja zaidi ya 20,000.
Mafanikio hayo yametajwa katika taarifa ya utendaji kazi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, iliyozinduliwa hivi karibuni, na kuonesha uimara wa mamlaka hiyo katika sekta ya maji na usafi wa mazingira.
Uzinduzi wa taarifa hiyo umefanywa na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa H. Aweso (Mb), ambaye amepongeza juhudi za mamlaka mbalimbali za maji nchini kwa kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa mafanikio ya SOUWASA kwa mwaka wa pili mfululizo ni ishara ya uthabiti wa kiutendaji na dhamira ya dhati ya kuwahudumia wananchi kwa viwango bora.
Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), utendaji wa mamlaka za maji hupimwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa huduma kwa wateja, ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, upatikanaji wa majisafi na salama, pamoja na usimamizi madhubuti wa miundombinu ya maji na majitaka.
SOUWASA imefanikiwa kufanya vizuri katika maeneo haya, jambo lililochangia kupanda kwa hadhi yake kitaifa.


Post a Comment