Kikao hicho kilichofanyika leo tarehe 5 Machi 2026, Kibaha, mkoani Pwani, kilihusisha Makatibu Wakuu wa Vyama 6 vya Ukombozi Kusini mwa Afrika, ambavyo ni ANC (Afrika Kusini), CCM (Tanzania), FRELIMO (Msumbiji), SWAPO (Namibia), ZANU-PF (Zimbabwe) na MPLA (Angola).
Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Asha-Rose Migiro, amesema kuwa katika kikao hicho wamepitia maazimio ya Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Vyama hivyo uliofanyika mwaka jana, nchini Afrika ya Kusini.
Amesema mijadala ilijikita kuangalia hali ya kisiasa katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, hususan kulinda uhuru wa kisiasa na kiuchumi, kutathmini malengo ya harakati za ukombozi pamoja na kuendelea kulinda na kuimarisha uhuru uliopatikana.
Dkt. Migiro amesema jukumu kubwa la vyama hivyo ni kuimarisha mshikamano na umoja wao pamoja na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili kanda hiyo ikiwemo mabadiliko ya tabianchi. Aidha, walijadili namna ya kutatua migogoro katika nchi wanachama na kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Katika kikao hicho pia walifanya mapitio ya maendeleo yaliyopatikana katika nchi zao, ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za jamii, kuboresha miundombinu pamoja na kuweka mikakati ya kujenga uchumi stahimilivu na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na umuhimu wa kuongeza ajira kwa vijana, kuwawezesha wanawake pamoja na kujenga uchumi jumuishi na stahimilivu kwa maendeleo ya Ukanda wa Kusini mwa Afrika.




إرسال تعليق