
Na Mbuke Shilagi, Kagera
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, amepiga marufuku uendeshaji wa disko toto katika kipindi cha sikukuu za Idd na Pasaka, akitaka shughuli hizo kusitishwa mara moja.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 19, 2026, Kamanda Chatanda amesema kuwa katika Mkoa wa Kagera hairuhusiwi kuandaa disko toto, na hadi sasa hawajapokea maombi yoyote kutoka kwa mtu au kikundi kinachotaka kuendesha shughuli hiyo.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha hawaachi nyumba bila uangalizi, pamoja na kuwasimamia watoto wao ili wasitembee barabarani peke yao bila mtu mzima.
Kwa upande wa madereva wa vyombo vya moto, ameonya vikali dhidi ya kuendesha wakiwa wamelewa, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kunahatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
Vilevile, Kamanda Chatanda amewapongeza waumini wa dini ya Kiislamu kwa kumaliza salama mfungo wa Ramadhani, na Wakristo wanaoelekea kumaliza mfungo wa Kwaresma.


إرسال تعليق