
Na Regina Ndumbaro Tunduru-Ruvuma
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratus Ndejembi, amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ya kukagua maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa laini ya kusafirisha umeme kutoka Songea kuelekea Tunduru na baadaye mikoa ya Lindi na Mtwara .
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Machi 7,2026, Waziri Ndejembi amesema mradi huo wa umeme wa kilovolti 220 (220KV) unalenga kuiunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika gridi ya taifa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na shughuli za kiuchumi hivyo serikali haitakubari kuona ujenzi wake unasuasua kutokana na uzembe wa mkandarasi.
Hata hivyo, Waziri Ndejembi ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kampuni ya Calvatal kuongeza juhudi mara moja, amesema licha ya kulipwa fedha mwezi Disemba, 2026, mkandarasi huyo hajarejea eneo la mradi kama walivyokubaliana walipokutana Dodoma.
"Kutokana na hali hii, ninamwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kutoa barua ya onyo kwa kampuni hiyo na kuitaka ndani ya wiki mbili iwe imerejea kikamilifu eneo la kazi na kuendelea na ujenzi, serikali haitavumilia ucheleweshaji wa miradi yote ya kimkakati lengo ni kuwasogezea wananchi huduma Bora na kwa wakati" Ameongeza.
Amesema kwa sasa mikoa ya Lindi na Mtwara bado inategemea umeme unaozalishwa ndani ya mkoa wa Lindi kupitia gesi, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uhakika wa umeme katika maeneo hayo.
Mhe. Ndejembi amesma laini hiyo inapita Songea na Tunduru huku serikali ikiwa imepanga kujenga kituo kikubwa cha kupoozea umeme (substation) kitakachoshusha umeme hadi kilovolti 33 kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa Tunduru, ambako kuna mahitaji makubwa ya umeme kutokana na uwepo wa rasilimali za madini na uwekezaji wa viwanda.
Mradi huo ulianza mwishoni mwa mwaka 2024 na ulitarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026, ambapo hadi sasa umefikia takribani asilimia 50 ya utekelezaji.
Gharama ya ujenzi wa laini kutoka Songea hadi Tunduru ni shilingi bilioni 516, huku kipande cha Tunduru hadi Masasi na Maumbika kikigharimu shilingi bilioni 316.
Aidha, serikali imetenga shilingi bilioni 5.7 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.
Waziri Ndejembi amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali kuhakikisha umeme unaozalishwa katika vituo mbalimbali ikiwemo Julius Nyerere Hydropower Plant, Mtera Dam, Kihansi Hydropower Plant na Kidatu Hydropower Plant unafika katika kila wilaya na mkoa kupitia gridi ya taifa.





Post a Comment